Ndugu Waandishi wa Habari,tumekuombeni mjumuike nasi siku ya leo ili kupitia ninyi, tuwafahamishe watanzania kuhusu mauzo ya awali ya hisa za benki yetu ya Mkombozi.Pamoja na kuwafahamisha lakini pia tutumie fursa hii kuwaomba watanzania washiriki katika ununuzi wa hisa za Benki ya Mkombozi.

 

Mauzo ya awali ya hisa husimamiwa na Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) na Mamlaka imekwishatoa idhini kwa Benki ya Mkombozi kukamilisha hatua hii ya uuzaji hisa za Benki kwa wananchi (IPO).

 

Zoezi hili litaanza Jumatatu tarehe 3 Novemba,2014 na kuishia Jumamosi,tarehe 29 Novemba,2014.Jumla ya hisa 5,000,000 zitauzwa kwa bei ya shilingi 1,000 kwa kila hisa.Hisa zitauzwa kupitia kwa madalali wote wa hisa,matawi yote ya benki ya Mkombozi na matawi yote ya benki ya CRDB.

 

Kuzinduliwa kwa mauzo haya (IPO) kunatoa nafasi kwa watanzania wote kuwekeza katika Benki ya Mkombozi ambayo inakua kwa kasi.

UTENDAJI WA BENKI TOKA IANZE (BANK PERFORMANCE)

 

Benki ya Mkombozi ilifungua milango kwa ajili ya kufanya biashara mnamo tarehe 28 Agosti 2009 ikiwa na tawi moja ambalo ni St. Joseph.Tangu kuanza kwake,Benki imekuwa ikifanya kazi kwa ufanisi na katika mwaka wake wa tatu (2011) Benki iliweza kupata faida.

 

Kutokana na kuridhishwa na utendaji wa Benki ya Mkombozi,Benki Kuu ya Tanzania iliweza kutoa idhini ya kufunguliwa matawi mengine matatu katika mwaka 2012.Matawi yaliyofunguliwa ni tawi la Mwanza, Msimbazi na Kariakoo.

 

Katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2013,benki ilipata faida ya shilingi 119.02 milioni.Katika mwaka huu wa 2014,benki inaendelea kukua kwa kasi kubwa.Kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2014 benki ilipata faida ya shilingi milioni 565.Hadi kufikia tarehe 30 Septemba benki imerekodi faida ya shilingi bilioni 1.04.

 

Kulingana na makisio yalipo katika Mpango wa Maendeleo wa Benki (Corporate Plan) kwa sasa,mtaji wa benki utafikia shilingi bilioni 21.94 tarehe 31 Desemba 2014, shilingi bilioni 24.95 tarehe 31 Desemba 2015 na shilingi bilioni 29.40 tarehe 31 Desemba 2014.

SABABU ZA UUZAJI WA HISA (IPO)

 

Kutokana na ukuaji huu wa kasi wa Benki,tumeona ni vema tupanue wigo wa umiliki wa benki na hivyo kufanya watanzania wengi zaidi wanufaike na ukuaji huu.Hivyo uuzaji huu wa hisa kupitia IPO:

 

  • Utatoa nafasi kwa Benki ya Mkombozi kukua zaidi na hivyo kuzidi kunufaisha wamiliki/wanahisa wake
  • Utawezesha Benki kufikia na kuvuka kiwango cha chini cha Mtaji (minimum capital requirement) kilichowekwa na Benki kuu ya Tanzania

Kulingana na miongozo ya Benki kuu,kiwango cha chini cha mitaji (minimum capital requirement ) kitaongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 15 kuanzia Machi,2015.Hata hivyo,hadi kufikia tarehe 30 Septemba 2014 tayari mtaji(Paid Up Capital) wetu ulifikia shilingi bilioni 16.84.

 

MATARAJIO YA BAADAYE

 

Benki ya Mkombozi itaweka mkazo kwenye maeneo muhimu ili kuongeza mapato ya benki na kufanya Benki iendelee kukua kwa kasi.Maeneo ambayo benki itatilia mkazo ni yale yatakayoongeza mapato,mali za Benki pamoja na wigo wa soko (market share) Maeneo haya ni pamoja na:

 

  • Uboreshaji wa huduma kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia
  • Kuanzisha huduma ya uwakala wa benki (agency banking) na uanzishwaji wa matawi (pale inapolazimu) ili kusogeza huduma karibu zaidi na wateja
  • Kuongesa deposits
  • Kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo ya wajasiriamali,mikopo ya makampuni,mikopo ya wafanyakazi, kuongeza ufunguaji wa akaunti

 MWISHO

Nachukua nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu kuchangamkia fursa hii kwa kununua hisa katika Benki yetu ya Mkombozi tena kwa bei ya chini kabisa (Shilingi 1000 tu).Naomba nisisitize pia kwamba muda uliotolewa na Mamlaka ni mfupi na ni muhimu tukazingatia hili ili tusipoteze fursa iliyopo mbele yetu.

Kama nilivyoeleza awali,ukuaji wa Benki kwa sasa ni mzuri mno na hivyo ninawaomba watanzania wenzangu tushiriki kikamilifu katika zoezi hili ili tufurahie matunda ya ukuaji benki kwa pamoja.Ni muhimu kufahamu kwamba baada ya zoezi hili (IPO) kumalizika,gharama za ununuzi wa hisa zitakuwa kubwa na jambo hili linaweza kukufanya usiweze kununua idadi ya hisa ambazo ungependa kununua katika benki ya Mkombozi.

Ninawashukuru sana kwa kunisikiliza.

 

Masha J Mshomba

MWENYEKITI