Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara Mkombozi inapenda kuwatangazia wanahisa wake kwamba zoezi la kuuza Hisa Nyongeza kwa wanahisa wake (‘Rights Issue’) imeongezewa muda mpaka tarehe 02/03/2021. Muda huu umeongezwa kutokana na maombi na maoni ya wanahisa wengi ambao hawakuweza kukamilisha taratibu za ununuzi wa Hisa Nyongeza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kilichotolewa hapo awali. Tunawasihi wale wote ambao hawakufanikiwa kununua Hisa Nyongeza wafanye hivyo ndani ya muda huu wa nyongeza. Lengo ni lile lile la kuiwezesha benki kuongeza mtaji kwa kiasi cha shilingi bilioni kumi na tano (TZS 15bn) ambao utasaidia kufanikisha uwekezaji katika upanuzi wa Benki na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia matawi wakala na miundombinu ya tehama.

Maelekezo na Masharti ya Ununuaji wa Hisa

  1. Wanaostahili kushiriki ni wanahisa ambao walikuwepo kwenye orodha ya wanahisa wa Benki mpaka kufikia tarehe 10/11/2020.
  2. Kila mwanahisa ana haki ya kununua Hisa Nyongeza sawa na idadi aliyo nayo kwa sasa kwenye Benki (mfano; mwenye Hisa 1,000 ana haki ya kununua Hisa nyingine 1,000 za nyongeza, n.k).
  3. Kila Hisa Nyongeza itauzwa kwa bei ya Tsh 750/=, ikiwa ni punguzo la asilimia ishirini na tano (25%) ya thamani ya hisa kwenye vitabu.
  4. Mwanahisa ambaye hatachukua haki yake ya Hisa Nyongeza au ambaye atanunua Hisa Nyongeza pungufu ya hisa anazomiliki atakuwa amepoteza haki hiyo au sehemu ya haki hiyo na hivyo watapewa wanahisa watakaoomba Hisa Nyongeza zaidi ya hisa wanazomiliki. 
  5. Hisa Nyongeza zitauzwa katika Matawi ya Benki ya Mkombozi na Benki ya Biashara Posta. Nakala za vitabu vya muamala zinapatikana katika matawi hayo na pia kwenye tovuti ya Benki ya Mkombozi (www.mkombozibank.co.tz)
  6. Tafadhali fika na nyaraka zifuatazo wakati wa ununuzi wa Hisa Nyongeza:

a) Cheti cha Hisa kinachoonyesha umiliki wako wa hisa za Benki ya Mkombozi au

b) CDS namba uliyopewa na Soko la Hisa.

  1.  Zoezi la uuzaji wa hisa nyongeza litafungwa rasmi tarehe 02/03/2021

Kwa taarifa zaidi kuhusu taratibu za ununuzi wa Hisa Nyongeza, mwanahisa anaweza kuwasiliana nasi kwa njia ya simu kwa huduma namba:- 0800 750 040 au barua pepe:-info@mkombozibank.co.tz. Anaweza pia kutembelea tawi lolote la benki ya Mkombozi lililopo karibu naye.

LIMETOLEWA NA;

Professor Marcellina Chijoriga,                                        Respige Onesmo Kimati,

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.                         Mkurugenzi Mtendaji.