TAARIFA KWA UMMA

23/12/2020.

Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya Biashara Mkombozi inakanusha taarifa ya kupotosha umma inayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kama ifuatavyo: -

Sio kweli kwamba Benki ya Mkombozi iko mbioni kufilisika. Kwa kipindi cha miaka kumi na moja (11) tangu kuanzishwa kwa Benki hii, Benki imepata mafanikio makubwa ambayo ni ya kujivunia. Hii ni pamoja na upanuzi wa huduma zake kwa kufungua matawi kumi na moja (11) hadi sasa. Benki pia imeendelea kufanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali za uwekezaji na utoaji huduma unaopelekea ufanisi katika vigezo muhimu vya utendaji kama vile kukua kwa mali za benki mwaka hadi mwaka kufikia shilingi bilioni 220; Amana za Wateja kufikia shilingi bilioni 180; Ukwasi wa Benki kufikia 31.5% na Mtaji msingi shilingi bilioni 9.37. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya utendaji ya mpaka mwisho wa Mwezi wa Novemba, 2020. Aidha, Benki ya Biashara ya Mkombozi inaendeshwa kwa kuzingatia vigezo vyote muhimu vya uendeshaji wa biashara ya benki na pale ambapo kuna dosari wakati wote mikakati na hatua mahususi za kutatua changamoto zimekuchuliwa. Benki Kuu ya Tanzania ambayo ndiyo taasisi yenye dhamana ya kusimamia shughuli za kibenki Tanzania imekuwa ikitekeleza kwa weledi wajibu wake wa kuisimamia Benki ya Biashara ya Mkombozi.

Mafanikio haya ya Benki yaliyoainishwa hapo juu ndiyo yaliyoipelekea Benki kutangaza gawio kwa wanahisa la kiasi cha shilingi milioni 412 mwaka 2016 na shilingi milioni 515 mwaka 2017. Hata hivyo, Benki inatambua kwamba mpaka sasa kuna wanahisa ambao bado hawajajitokeza kuchukua gawio lao. Juhudi za kuwafikia zimefanyika ikiwemo kutoa wito huo kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kupitia tovuti ya Benki. Benki imeendelea kusimamia fedha za gawio hilo na kuzitolea taarifa kwa mujibu wa sheria na miongozo ya mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA). Ifahamike kwamba kutoa gawio kwa wawekezaji kunazingatia upatikanaji wa faida ya kutosha na vipaumbele vya uwekezaji wa taasisi husika na vivyo hivyo kwa Benki ya Biashara ya Mkombozi.

Benki ya Biashara ya Mkombozi inaendeshwa na Bodi na Menejimenti zenye wajumbe wenye weledi mkubwa katika nyanja mbali mbali na muhimu katika uendeshaji wa taasisi ya kibenki. Hii ni pamoja na nyanja za Fedha, Uendeshaji wa Biashara, Uhasibu, Sheria, Tehama na uzoefu wa utendaji katika taasisi mbalimbali za kibenki na zisizo za kibenki. Wajumbe hawa wanakidhi vigezo vyote muhimu vya kisheria vinavyosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania. Tunapenda kuhakikishia umma wa Wanahisa, Wateja na Wadau wote wa Benki ya Biashara ya Mkombozi kuwa benki hii inaendeshwa kwa weledi mkubwa katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na utoaji mikopo ambao unazingatia kanuni na masharti yanayosimamia biashara ya kibenki.

Tunapenda kuwafahamisha umma kwa ujumla kwamba taarifa za mahesabu ya Benki zimekuwa mara zote zikikaguliwa na mojawapo ya taasisi nne kuu na bobezi katika ukaguzi wa mahesabu duniani. Kwa kipindi cha miaka kumi na moja (11) tangu kuanzishwa kwa Benki hii, Benki haijawahi kupata hati chafu kutoka katika kaguzi zote zinazofanyika kila mwaka. Hivyo basi, ni rai yetu kwa umma kuendelea kuwa na imani na taarifa za hesabu zinazotolewa na Benki kwani ni taarifa sahihi zilizokaguliwa na Wakaguzi wa ndani, nje na Benki Kuu. Taarifa hizi zinaonyesha hali halisi ya uendeshaji wa Benki katika vipindi tofauti kama zilivyokaguliwa.

Aidha, katika kuhakikisha ukuaji na kuongeza ufanisi wa biashara, Benki ya Biashara ya Mkombozi imeandaa mpango mkakati wa kuongeza mtaji wake ili kufanikisha uwekezaji kwenye upanuzi na huduma zake ili kuwafikia wananchi wengi hasa wa vijijini. Benki iko mbioni kufungua dirisha la kukusanya mtaji nyongeza kutoka kwa wanahisa wake ili kufanikisha mkakati uliokusudiwa kiuwekezaji.

Mwisho, Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara ya Mkombozi inapenda kuwahakikishia Wanahisa, Wateja na Wadau wote kwamba Benki iko imara na inaendelea kutoa huduma kwa wananchi kama kawaida katika matawi yake yote nchini.

Kwa maelezo zaidi tafadhali wasiliana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi.


Professor Marcellina Chijoriga.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.